James 4

Jinyenyekezeni Kwa Mungu

1 aNi kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2 bMnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 cMnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

4 dNinyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. 5 eAu mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6 fLakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema: “Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

7 gBasi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 hMkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9 iHuzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10 jJinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.

Onyo Kuhusu Kuhukumu Wengine

11 kNdugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu yeyote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria. 12 lYuko Mtoa sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu, ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?

Kujivuna Kwa Ajili Ya Kesho

13 mBasi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 nLakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 oBadala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 pKama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 qBasi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
Copyright information for SwhKC